‏ Song of Solomon 3

1Usiku kucha kwenye kitanda changu
nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye;
nilimtafuta, lakini sikumpata.
2Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini,
katika barabara zake na viwanja;
nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye.
Kwa hiyo nilimtafuta lakini sikumpata.
3Walinzi walinikuta
walipokuwa wakizunguka mji.
Nikawauliza, “Je, mmemwona
yule moyo wangu umpendaye?”
4Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita
nilimpata yule moyo wangu umpendaye.
Nilimshika na sikumwachia aende
mpaka nilipomleta katika nyumba ya mama yangu,
katika chumba cha yule aliyenichukua mimba.
5Binti za Yerusalemu, ninawaagiza
kwa paa na kwa ayala wa shambani:
Msichochee wala kuamsha mapenzi
hata yatakapotaka yenyewe.

Shairi La Tatu

Mpenzi 6Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani
kama nguzo ya moshi,
anayenukia manemane na uvumba
iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote
vya mfanyabiashara?
7Tazama! Ni gari la Solomoni
lisindikizwalo na mashujaa sitini,
walio wakuu sana wa Israeli,
8wote wamevaa panga,
wote wazoefu katika vita,
kila mmoja na upanga wake pajani,
wamejiandaa kwa ajili ya hofu za usiku.
9Mfalme Solomoni alijitengenezea gari;
alilitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni.
10Nguzo zake alizitengeneza kwa fedha,
kitako chake kwa dhahabu.
Kiti chake kilipambwa kwa zambarau,
gari lake likanakshiwa njumu kwa upendo
na binti za Yerusalemu.
11Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni,
mkamtazame Mfalme Solomoni akiwa amevaa taji,
taji ambalo mama yake alimvika
siku ya arusi yake,
siku ambayo moyo wake ulishangilia.
Copyright information for SwhNeno