‏ 2 Chronicles 11:5-23

Yeroboamu Ajengea Yuda Ngome

5Rehoboamu akaishi Yerusalemu akajenga miji yenye ngome katika Yuda: 6Akajenga Bethlehemu, Etamu, Tekoa, 7Beth-Suri, Soko, Adulamu, 8Gathi, Maresha, Zifu, 9Adoraimu, Lakishi, Azeka, 10Sora, Aiyaloni na Hebroni. Hii ndiyo iliyokuwa miji iliyojengewa ngome katika Yuda na Benyamini. 11Akaimarisha ulinzi wake na kuweka majemadari ndani yake, pamoja na ghala za mahitaji ya vyakula, mafuta ya zeituni na divai. 12Akaweka ngao na mikuki katika miji na kuifanya iwe imara sana. Kwa hiyo Yuda na Benyamini zikawa zake.

13Makuhani na Walawi kutoka sehemu zote za Israeli wakawa upande wake. 14Pia Walawi wakaacha maeneo yao ya malisho na mali zao, wakaja Yuda na Yerusalemu kwa sababu Yeroboamu na wanawe walikuwa wamewakataa wasiwe makuhani wa Bwana. 15Naye akawa amechagua makuhani wake mwenyewe kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia sanamu za mbuzi na za ndama ambazo alikuwa ametengeneza. 16Wale waliotoka katika kila kabila la Israeli ambao walielekeza mioyo yao kumtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, wakawafuata Walawi huko Yerusalemu kumtolea Bwana dhabihu, Mungu wa baba zao. 17Wakaimarisha ufalme wa Yuda na kumuunga mkono Rehoboamu mwana wa Solomoni miaka mitatu, wakienenda katika njia za Daudi na Solomoni katika wakati huu.

Jamaa Ya Rehoboamu

18Rehoboamu alimwoa Mahalati ambaye alikuwa binti Yeremothi mwana wa Daudi, mamaye alikuwa Abihaili binti Eliabu mwana wa Yese. 19Mahalati alimzalia Rehoboamu wana: Yeushi, Shemaria na Zahamu. 20Kisha akamwoa Maaka binti Absalomu, ambaye alimzalia: Abiya, Atai, Ziza na Shelomithi. 21Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu zaidi kuliko wakeze wengine na masuria wake. Kwa jumla alikuwa na wake kumi na wanane na masuria sitini, wana ishirini na wanane na binti sitini.

22Rehoboamu akamweka Abiya mwana wa Maaka, kuwa mkuu wa wana wa mfalme miongoni mwa ndugu zake ili amfanye mfalme. 23Akatenda kwa busara, akiwasambaza baadhi ya wanawe katika wilaya zote za Yuda na Benyamini, pamoja na miji yote yenye ngome. Akawapa mahitaji tele na kuwaoza wake wengi.

‏ 2 Chronicles 12:1-15

Shishaki Ashambulia Yerusalemu

(1 Wafalme 14:25-28)

1Baada ya nafasi ya Rehoboamu kuimarika na kuwa na nguvu, yeye na Israeli yote waliiacha sheria ya Bwana Mungu. 2Kwa sababu hawakuwa waaminifu kwa Bwana, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu. 3Akiwa na magari ya vita 1,200 na wapanda farasi 60,000 na idadi isiyohesabika ya majeshi ya Walibia, Wasukii na Wakushi
Yaani watu kutoka sehemu ya Naili ya juu.
yaliyokuja pamoja naye kutoka Misri.
4Akateka miji ya Yuda yenye ngome akaendelea mpaka Yerusalemu.

5Ndipo nabii Shemaya akaja kwa Rehoboamu na kwa viongozi wa Yuda waliokuwa wamekusanyika huko Yerusalemu kwa ajili ya hofu ya Shishaki naye akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, ‘Ninyi mmeniacha mimi, kwa hiyo, mimi nami sasa ninawaacha ninyi mkononi mwa Shishaki.’ ”

6Viongozi wa Israeli na mfalme wakajinyenyekeza na kusema, “Bwana Mungu ni mwenye haki.”

7 Bwana Mungu alipoona kwamba wamejinyenyekeza, neno hili la Bwana likamjia Shemaya: “Maadamu wamejinyenyekeza, sitawaangamiza bali hivi karibuni nitawapatia wokovu. Ghadhabu yangu haitamwagwa juu ya Yerusalemu kwa kupitia Shishaki. 8Hata hivyo, watamtumikia Shishaki ili wapate kujifunza tofauti kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa nchi nyingine.”

9Shishaki mfalme wa Misri alipoishambulia Yerusalemu, alichukua hazina za Hekalu la Bwana na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao za dhahabu ambazo Solomoni alikuwa amezitengeneza. 10Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme. 11Kila wakati mfalme alipokwenda katika Hekalu la Bwana walinzi walikwenda pamoja naye wakiwa wamebeba hizo ngao na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.

12Kwa sababu Rehoboamu alijinyenyekeza, hasira ya Bwana ikageukia mbali naye, hakuangamizwa kabisa. Kukawa na hali nzuri katika Yuda.

13Mfalme Rehoboamu akajiweka imara katika Yerusalemu na akaendelea kuwa mfalme. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na saba, mji ambao Bwana alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili aliweke Jina lake humo. Mama yake aliitwa Naama, alikuwa Mwamoni. 14Rehoboamu akatenda maovu kwa sababu hakuuelekeza moyo wake katika kumtafuta Bwana Mungu.

15Kwa habari ya matukio katika utawala wa Rehoboamu, tangu mwanzo mpaka mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Shemaya na mwonaji Ido zinazohusiana na vizazi? Kulikuwako na vita mara kwa mara kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.
Copyright information for SwhNeno