‏ 2 Samuel 6:12-22

12Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, “Bwana ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu.” Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe. 13Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Bwana walipokuwa wametembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa. 14Daudi, akiwa amevaa kisibau cha kitani, alicheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote, 15wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la Bwana kwa shangwe na sauti za tarumbeta.

16Ikawa Sanduku la Bwana lilipokuwa linaingia katika Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za Bwana, akamdharau moyoni mwake.

17Wakaleta Sanduku la Bwana na kuliweka mahali pake ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana. 18Baada ya kumaliza kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, Daudi akawabariki watu katika jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote. 19Kisha akatoa mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu kwa kila mtu katika mkutano wote wa Waisraeli, wanaume kwa wanawake. Nao watu wote wakaenda nyumbani kwao.

20Daudi aliporudi ili kuwabariki watu wa nyumbani mwake, Mikali binti Sauli akatoka nje kumlaki, akamwambia, “Tazama jinsi mfalme wa Israeli alivyojibainisha mwenyewe leo kwa kuvua mavazi yake machoni pa vijakazi wa watumishi wake, kama vile ambavyo mtu asiye na adabu angelifanya!”

21Daudi akamwambia Mikali, “Nilifanya hivyo mbele za Bwana ambaye alinichagua mimi badala ya baba yako au mwingine yeyote kutoka nyumba yake wakati aliponiweka niwe mtawala juu ya Israeli, watu wa Bwana. Kwa hiyo nitacheza mbele za Bwana. 22Nitakuwa asiye na heshima zaidi kuliko sasa, nami nitajishusha machoni pangu mwenyewe. Lakini kwa hawa vijakazi uliosema habari zao nitaheshimiwa.”
Copyright information for SwhNeno