2 Samuel 7:1-17
Ahadi Ya Mungu Kwa Daudi
(1 Nyakati 17:1-15)
1Baada ya mfalme kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, naye Bwana akiwa amemstarehesha pande zote mbali na adui zake, 2akamwambia nabii Nathani, “Mimi hapa, ninaishi katika jumba la kifalme la mierezi, wakati Sanduku la Mungu limebaki katika hema.” 3Nathani akamjibu mfalme, “Lolote ulilo nalo moyoni, endelea ukalifanye, kwa maana Bwana yu pamoja nawe.” 4Usiku ule neno la Bwana likamjia Nathani, kusema: 5“Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Je, ewe ndiwe wa kunijengea mimi nyumba ili nikae ndani yake? 6Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine ndani ya hema kama makao yangu. 7Popote nilipotembea pamoja na Waisraeli wote, je, nimewahi kumwambia kiongozi wao yeyote niliyemwamuru kuwachunga watu wangu Israeli, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?” ’ 8“Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: Nilikutoa wewe kutoka machungani na kutoka kuandama kundi la kondoo na mbuzi ili kuwaongoza watu wangu Israeli. 9Nimekuwa pamoja nawe popote ulipokwenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani. 10Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili kwamba wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya mwanzoni, 11na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa raha mbele ya adui zenu wote. “ ‘Bwana akuambia kwamba Bwana mwenyewe atakujengea nyumba. 12Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, ambaye atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. 13Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, nami nitaimarisha kiti cha enzi cha ufalme wake milele. 14Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapokosea nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu, kwa adhabu ya kupigwa na wanadamu. 15Lakini upendo wangu kamwe hautaondolewa kwake, kama nilivyouondoa kwa Sauli, niliyemwondoa atoke mbele yako. 16Nyumba yako na ufalme wako utadumu milele mbele zangu, kiti chako cha enzi kitafanywa imara milele.’ ” 17Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.
Copyright information for
SwhNeno