‏ Deuteronomy 28:1-14

Baraka Za Utiifu

(Walawi 26:3-13; Kumbukumbu 7:12-24)

1Kama ukimtii Bwana Mungu wako kwa bidii na kufuata amri zake zote ninazokupa leo kwa bidii, Bwana Mungu wako atakuweka juu ya mataifa yote katika dunia. 2Baraka hizi zote zitakuja juu yako na kukupata, kama ukimtii Bwana Mungu wako:

3Utabarikiwa mjini na utabarikiwa mashambani.

4Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na mazao ya nchi yako na wanyama wako wachanga wa kufugwa, yaani ndama wa makundi yako ya ngʼombe, na wana-kondoo wa makundi yako.

5Kapu lako na vyombo vyako vya kukandia vitabarikiwa.

6Utabarikiwa uingiapo na utabarikiwa utokapo.

7 Bwana atasababisha adui wainukao dhidi yako kushindwa mbele yako. Watakujia kwa njia moja lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.

8 Bwana ataagiza baraka juu ya ghala zako na juu ya kila kitu utakachogusa kwa mkono wako. Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi anayokupa.

9 Bwana atakufanya kuwa taifa lake takatifu, kama alivyokuahidi kwa kiapo, kama ukishika maagizo ya Bwana Mungu wako na kwenda katika njia zake. 10Kisha mataifa yote ya dunia wataona kuwa unaitwa kwa jina la Bwana, nao watakuogopa. 11Bwana atakupa kustawi kwa wingi, katika tunda la uzao wa tumbo lako, katika wanyama wachanga wa mifugo yako na katika mazao ya ardhi yako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwapa.

12 Bwana atafungua mbingu, ghala zake za baraka, kukupa mvua kwa majira yake na kubariki kazi zako zote za mikono yako. Utakopesha mataifa mengi lakini hutakopa kwa yeyote. 13Bwana atakufanya kichwa, wala si mkia. Kama utazingatia maagizo ya Bwana Mungu wako ninayokupa siku hii ya leo na kuyafuata kwa bidii, daima utakuwa juu, kamwe hutakuwa chini. 14Usihalifu amri zangu zozote ninazokupa leo, kwa kwenda kuume au kushoto, kwa kufuata miungu mingine na kuitumikia.
Copyright information for SwhNeno