Exodus 31:1-11
Bezaleli Na Oholiabu
(Kutoka 35:30–36:1)
1Ndipo Bwana akamwambia Mose, 2“Tazama, nimemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, 3nami nimemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi, 4ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, 5kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi. 6Tena nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, ili kumsaidia. Pia mafundi wote nimewapa ustadi wa kutengeneza kila kitu nilichokuamuru wewe: 7Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda pamoja na kiti cha rehema juu yake, pia na vifaa vyote vya kwenye hema, 8meza na vifaa vyake, kinara cha taa cha dhahabu safi na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, 9madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, sinia na kinara chake, 10pamoja na mavazi matakatifu yaliyofumwa ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe wakati wanahudumu katika kazi ya ukuhani, 11pia mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri kwa ajili ya Mahali Patakatifu. Watavitengeneza sawasawa kama vile nilivyokuagiza wewe.”
Copyright information for
SwhNeno