‏ Isaiah 37:21-38

Kuanguka Kwa Senakeribu

(2 Wafalme 19:20-37)

21Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Kwa sababu umeniomba kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru, 22hili ndilo neno ambalo Bwana amelisema dhidi yake: “Bikira binti Sayuni anakudharau na kukudhihaki.
Binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake unapokimbia.
23Ni nani uliyemtukana na kumkufuru?
Ni nani uliyeinua sauti yako dhidi yake,
na kumwinulia macho yako kwa kiburi?
Ni dhidi ya yule Aliye Mtakatifu wa Israeli!
24Kupitia kwa wajumbe wako
umelundika matukano juu ya Bwana.
Nawe umesema,
‘Kwa magari yangu mengi ya vita,
nimepanda juu ya vilele vya milima,
vilele vya juu sana katika Lebanoni.
Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu,
misunobari yake iliyo bora sana.
Nimefikia sehemu zake zilizoinuka juu sana,
misitu yake iliyo mizuri sana.
25Nimechimba visima katika nchi za kigeni
na kunywa maji yake.
Kwa nyayo za miguu yangu
nimekausha vijito vyote vya Misri.’

26“Je, hujasikia?
Zamani sana niliamuru hili.
Siku za kale nilipanga hili;
sasa nimelifanya litokee,
kwamba umegeuza miji yenye ngome
kuwa malundo ya mawe.
27Watu wa miji hiyo wameishiwa nguvu,
wanavunjika mioyo na kuaibishwa.
Wao ni kama mimea katika shamba,
kama machipukizi mororo ya kijani,
kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba,
ambayo hukauka kabla ya kukua.

28“Lakini ninajua mahali ukaapo,
kutoka kwako na kuingia kwako,
na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu.
29Kwa sababu unaghadhibika na ufidhuli dhidi yangu,
na kwa sababu ufidhuli wako umefika masikioni mwangu,
nitaweka ndoana yangu puani mwako
na hatamu yangu kinywani mwako,
nami nitakufanya urudi kwa njia ile uliyoijia.

30“Hii ndiyo itakuwa ishara kwako, ee Hezekia: “Mwaka huu utakula kile kiotacho chenyewe,
na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake.
Lakini katika mwaka wa tatu panda na uvune,
panda mashamba ya mizabibu na ule matunda yake.
31Mara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda
wataeneza mizizi chini na kuzaa matunda juu.
32Kwa kuwa kutoka Yerusalemu watakuja mabaki,
na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika.
Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote,
ndio utatimiza jambo hili.

33“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana kuhusu mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu
wala hatapiga mshale hapa.
Hatakuja mbele yake na ngao
wala kupanga majeshi kuuzingira.
34Kwa njia ile aliyoijia ndiyo atakayorudi;
hataingia katika mji huu,”
asema Bwana.
35“Nitaulinda mji huu na kuuokoa,
kwa ajili yangu mwenyewe,
na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu!”

36Ndipo malaika wa Bwana akaenda, akawaua wanajeshi 185,000 katika kambi ya Waashuru. Wenzao walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali! 37Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Akarudi Ninawi na kukaa huko.

38Siku moja, alipokuwa akiabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza wakamuua kwa upanga, nao wakakimbilia nchi ya Ararati. Naye Esar-Hadoni mwanawe akawa mfalme badala yake.
Copyright information for SwhNeno