‏ Jeremiah 52:3-11

3Ilikuwa ni kwa sababu ya hasira ya Bwana haya yote yalitokea Yerusalemu na Yuda, naye mwishoni akawaondoa mbele zake.

Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli.

4Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akiwa na jeshi lake lote alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Wakapiga kambi nje ya mji na kuuzunguka mji pande zote. 5Mji ulizungukwa na jeshi mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia.

6Ilipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu. 7Kisha ukuta wa mji ukavunjwa na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba. 8Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia Mfalme Sedekia na kumpata katika sehemu tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika, 9naye akakamatwa.

Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mahali ambapo alimtangazia hukumu.
10Huko Ribla mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Pia akawaua maafisa wote wa Yuda. 11Kisha akayangʼoa macho ya Sedekia, akamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli, alipomweka gerezani mpaka siku ya kifo chake.
Copyright information for SwhNeno