‏ John 18:33-40

33Kwa hiyo Pilato akaingia ndani ya jumba la kifalme, akamwita Yesu, akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

34Yesu akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe, au uliambiwa na watu kunihusu mimi?”

35Pilato akamjibu, “Mimi si Myahudi, ama sivyo? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?”

36Yesu akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini kama ilivyo, ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.”

37Pilato akamuuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Yesu akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa, na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Mtu yeyote aliye wa kweli husikia sauti yangu.”

38Pilato akamuuliza Yesu, “Kweli ni nini?” Baada ya kusema haya Pilato akaenda nje tena akawaambia wale viongozi wa Wayahudi waliomshtaki Yesu, “Sioni kosa lolote alilotenda mtu huyu. 39Lakini ninyi mna desturi yenu kwamba wakati wa Pasaka nimwachie huru mfungwa mmoja mnayemtaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi’?”

40Wao wakapiga kelele wakisema, “Si huyu mtu, bali tufungulie Baraba!” Yule Baraba alikuwa mnyangʼanyi.

‏ John 19:1-16

Yesu Ahukumiwa Kusulubiwa

(Mathayo 27:15-31; Marko 15:6-20; Luka 23:13-25)

1Ndipo Pilato akamtoa Yesu akaamuru apigwe mijeledi. 2Askari wakasokota taji ya miiba, wakamvika Yesu kichwani. Wakamvalisha joho la zambarau. 3Wakawa wanapanda pale alipo tena na tena, wakisema, “Salamu! Mfalme wa Wayahudi!” Huku wakimpiga makofi usoni.

4Pilato akatoka tena nje akawaambia wale waliokusanyika, “Tazameni, namkabidhi Yesu kwenu kuwajulisha kwamba mimi sikumwona ana hatia.” 5Kwa hiyo Yesu akatoka nje akiwa amevaa ile taji ya miiba na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni, huyu hapa huyo mtu!”

6Wale viongozi wa makuhani na maafisa walipomwona, wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”

Pilato akawaambia, “Mchukueni ninyi mkamsulubishe, mimi sioni hatia juu yake.”

7Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria na kutokana na sheria hiyo, hana budi kufa kwa sababu yeye alijiita Mwana wa Mungu.”

8Pilato aliposikia haya, akaogopa zaidi. 9Akaingia tena ndani ya jumba la kifalme, akamuuliza Yesu, “Wewe umetoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu. 10Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulubisha?”

11Ndipo Yesu akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.”

12Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Yesu, lakini Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu yeyote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.”

13Pilato aliposikia maneno haya akamtoa Yesu nje tena akaketi katika kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe, kwa Kiebrania paliitwa Gabatha
Gabatha ni neno la Kiebrania ambalo maana yake ni Sakafu ya jiwe; ni mahali pa wazi palipoinuliwa ambako palitumika kama mahakama.
14Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi.

Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”

15Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!”

Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe mfalme wenu?”

Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.”

16Ndipo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili wamsulubishe.

Kusulubiwa Kwa Yesu

(Mathayo 27:32-44; Marko 15:21-32; Luka 23:26-43)

Kwa hiyo askari wakamchukua Yesu.
Copyright information for SwhNeno