‏ Leviticus 26:3-13

3“ ‘Ikiwa mtafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii maagizo yangu, 4nitawanyeshea mvua katika majira yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake. 5Kupura nafaka kwenu kutaendelea mpaka wakati wa kuvuna zabibu. Pia kuvuna zabibu kutaendelea mpaka wakati wa kupanda mbegu, nanyi mtakula na kushiba, na mtaishi salama katika nchi yenu.

6“ ‘Nitawapa amani katika nchi, mpate kulala pasipo kutiwa hofu na yeyote. Nitawaondoa wanyama wakali watoke kwenye nchi, nao upanga hautapita katika nchi yenu. 7Mtawafukuza adui zenu, nanyi mtawaua kwa upanga mbele yenu. 8Watu wenu watano watafukuza adui mia, watu wenu mia watafukuza adui elfu kumi, nao adui zenu wataanguka kwa upanga mbele yenu.

9“ ‘Nitawaangalia kwa upendeleo na kuwafanya mzae na kuzidisha idadi yenu, nami nitalishika Agano langu na ninyi. 10Wakati wa kuvuna mtakuwa bado mnakula mavuno ya mwaka uliopita, na itawalazimu kuyaondoa ghalani ili mpate nafasi ya mavuno mapya. 11Nitafanya makao yangu miongoni mwenu, nami sitawachukia. 12Nitatembea katikati yenu niwe Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu. 13Mimi ndimi Bwana Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili msiendelee kuwa watumwa wa Wamisri, nikavunja kongwa lenu, na kuwawezesha kutembea mkiwa mmeinua vichwa vyenu juu.
Copyright information for SwhNeno