‏ Luke 19:28-40

Yesu Aingia Yerusalemu Kwa Ushindi

(Mathayo 21:1-11; Marko 11:1-11; Yohana 12:12-19)

28Baada ya Yesu kusema haya, alitangulia kupanda kwenda Yerusalemu. 29Naye alipokaribia Bethfage na Bethania kwenye mlima uitwao Mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, 30“Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa. 31Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’ ”

32Wale waliotumwa wakaenda, wakakuta kila kitu kama vile Yesu alivyokuwa amewaambia. 33Walipokuwa wanamfungua yule mwana-punda, wenyewe wakawauliza, “Mbona mnamfungua huyo mwana-punda?”

34Wale wanafunzi wakajibu, “Bwana anamhitaji.”

35Wakamleta kwa Yesu, nao baada ya kutandika mavazi yao juu ya huyo mwana-punda, wakampandisha Yesu juu yake. 36Alipokuwa akienda akiwa amempanda, watu wakatandaza mavazi yao barabarani.

37Alipokaribia mahali yanapoanzia materemko ya Mlima wa Mizeituni, umati wote wa wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa furaha kwa sauti kuu kwa ajili ya matendo yote ya miujiza waliyoyaona. Wakasema: 38“Amebarikiwa Mfalme ajaye kwa Jina la Bwana!”
“Amani mbinguni na utukufu huko juu sana.”

39Baadhi ya Mafarisayo waliokuwamo miongoni mwa ule umati wa watu wakamwambia, “Mwalimu, waamuru wanafunzi wako wanyamaze.”

40Yesu akawajibu, “Nawaambia ninyi, kama hawa wakinyamaza, mawe yatapiga kelele.”
Copyright information for SwhNeno