Luke 21:7-19
Mateso
(Mathayo 24:3-14; Marko 13:3-13)
7Wakamuuliza, “Mwalimu, mambo haya yatatukia lini? Ni dalili gani itaonyesha kwamba yanakaribia kutendeka?” 8Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate. 9Lakini msikiapo habari za vita na machafuko, msiogope. Kwa maana hayo ni lazima yatokee kwanza, ila ule mwisho hautakuja wakati huo.” 10Kisha akawaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme mmoja dhidi ya ufalme mwingine. 11Kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, na njaa kali, na magonjwa ya kuambukiza katika sehemu mbalimbali. Pia kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni. 12 “Lakini kabla yote hayajatokea, watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawatia mikononi mwa wakuu wa masinagogi na kuwafunga magerezani. Nanyi mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya Jina langu. 13Hii itawapa nafasi ya kushuhudia. 14Lakini kusudieni mioyoni mwenu msisumbuke awali kuhusu mtakalosema mbele ya mashtaka. 15Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga. 16Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki, na baadhi yenu watawaua. 17Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. 18Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia. 19Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.
Copyright information for
SwhNeno