Luke 22:39-46
Yesu Aomba Kwenye Mlima Wa Mizeituni
(Mathayo 26:36-46; Marko 14:32-42)
39Yesu akatoka, akaenda kwenye Mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa kawaida yake, nao wanafunzi wake wakamfuata. 40Walipofika huko, akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni, msije mkaingia majaribuni.” 41Akajitenga nao kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba 42akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.” 43Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu. 44Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini. 45Baada ya kuomba, akawarudia wanafunzi wake akawakuta wamelala, wakiwa wamechoka kutokana na huzuni. 46Naye akawauliza, “Mbona mmelala? Amkeni, mwombe ili msije mkaingia majaribuni.”
Copyright information for
SwhNeno