Luke 4:1-13
Yesu Ajaribiwa Na Shetani
(Mathayo 4:1-11; Marko 1:12-13)
1Yesu, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akarudi kutoka Yordani. Akaongozwa na Roho Mtakatifu hadi nyikani, 2mahali ambako kwa siku arobaini alikuwa akijaribiwa na ibilisi. Kwa siku zote hizo hakula chochote, hivyo baada ya muda huo akaona njaa. 3Ibilisi akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.” 4Yesu akajibu akamwambia, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’ ” 5Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonyesha milki zote za dunia kwa mara moja. 6Akamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa yeyote ninayetaka. 7Hivyo ikiwa utanisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.” 8Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake.’ ” 9Kisha ibilisi akampeleka mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa, 10kwa maana imeandikwa: “ ‘Atakuagizia malaika zakeili wakulinde;
11nao watakuchukua mikononi mwao,
usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”
12Yesu akamjibu, “Imesemwa, ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ” 13Ibilisi alipomaliza kila jaribu, akamwacha Yesu mpaka wakati mwingine ufaao.
Copyright information for
SwhNeno