Luke 8:40-56
Msichana Afufuliwa, Na Mwanamke Aponywa
(Mathayo 9:18-26; Marko 5:21-43)
40Basi Yesu aliporudi, umati mkubwa wa watu ukampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea. 41Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Yesu, akimwomba afike nyumbani kwake, 42kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa. Yesu alipokuwa akienda, umati wa watu ukamsonga sana. 43Katika umati huo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna yeyote aliyeweza kumponya. 44Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Yesu na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma. 45Yesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?” Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.” 46Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.” 47Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Yesu. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara. 48Basi Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.” 49Yesu alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.” 50Yesu aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.” 51Walipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, pamoja na baba na mama wa yule binti. 52Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Yesu akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.” 53Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa. 54Yesu akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!” 55Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula. 56Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote juu ya yale yaliyotukia.
Copyright information for
SwhNeno