Mark 14:12-21
Yesu Ala Pasaka Na Wanafunzi Wake
(Mathayo 26:17-25; Luka 22:7-14, 21-23; Yohana 13:21-30)
12Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo kwa desturi mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wa Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?” 13Basi akawatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni mjini. Huko mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni. 14Mwambieni mwenye nyumba ile atakayoingia, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba changu cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ 15Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kilichopambwa tena kilicho tayari. Tuandalieni humo.” 16Wale wanafunzi wakaondoka na kwenda mjini, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka. 17Ilipofika jioni, Yesu akaja pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. 18Walipoketi mezani wakila, Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti, mmoja anayekula pamoja nami.” 19Wakaanza kuhuzunika na kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?” 20Akawajibu, “Ni mmoja miongoni mwenu ninyi kumi na wawili, yule anayechovya mkate kwenye bakuli pamoja nami. 21Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa.”
Copyright information for
SwhNeno