Mark 14:53-65
Yesu Mbele Ya Baraza La Wayahudi
(Mathayo 26:57-68; Luka 22:54-71; Yohana 18:13-24)
53Wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu, nao viongozi wa makuhani wote, na wazee na walimu wa sheria wote wakakusanyika pamoja. 54Petro akamfuata kwa mbali, hadi uani kwa kuhani mkuu. Huko akaketi pamoja na walinzi, akiota moto. 55Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi ▼▼Baraza la Wayahudi hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.
lote wakatafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote. 56Wengi walitoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana. 57Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema: 58“Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ” 59Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana. 60Basi kuhani mkuu akasimama mbele yao, akamuuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” 61Lakini Yesu akakaa kimya, hakusema neno lolote. Kuhani mkuu akamuuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, ▼▼Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
Mwana wa Mungu Aliyebarikiwa?” 62Yesu akajibu, “Mimi ndimi. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.” 63Kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? 64Ninyi mmesikia hayo makufuru. Uamuzi wenu ni gani?” Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo. 65Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi.
Copyright information for
SwhNeno