‏ Mark 14:53-72

Yesu Mbele Ya Baraza La Wayahudi

(Mathayo 26:57-68; Luka 22:54-71; Yohana 18:13-24)

53Wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu, nao viongozi wa makuhani wote, na wazee na walimu wa sheria wote wakakusanyika pamoja. 54Petro akamfuata kwa mbali, hadi uani kwa kuhani mkuu. Huko akaketi pamoja na walinzi, akiota moto.

55Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi
Baraza la Wayahudi hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.
lote wakatafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote.
56Wengi walitoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana.

57Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema: 58“Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ” 59Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana.

60Basi kuhani mkuu akasimama mbele yao, akamuuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” 61Lakini Yesu akakaa kimya, hakusema neno lolote.

Kuhani mkuu akamuuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo,
Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
Mwana wa Mungu Aliyebarikiwa?”

62Yesu akajibu, “Mimi ndimi. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

63Kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? 64Ninyi mmesikia hayo makufuru. Uamuzi wenu ni gani?”

Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo.
65Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi.

Petro Amkana Yesu

(Mathayo 26:69-75; Luka 22:56-62; Yohana 18:15-18, 25-27)

66Petro alipokuwa bado yuko chini kwenye ua wa jumba la kifalme, tazama akaja mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu. 67Alipomwona Petro akiota moto, akamtazama sana, akamwambia,

“Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

68Lakini Petro akakana, akasema, “Sijui wala sielewi unalosema.” Naye akaondoka kuelekea kwenye njia ya kuingilia.

69Yule mtumishi wa kike alipomwona mahali pale, akawaambia tena wale waliokuwa wamesimama hapo, “Huyu mtu ni mmoja wao.” 70Lakini Petro akakana tena.

Baada ya muda kidogo wale waliokuwa wamesimama hapo karibu na Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya!”
71Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui huyu mtu mnayesema habari zake!”

72Papo hapo jogoo akawika mara ya pili. Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alikuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Akavunjika moyo, akalia sana.
Copyright information for SwhNeno