‏ Mark 14:66-72

Petro Amkana Yesu

(Mathayo 26:69-75; Luka 22:56-62; Yohana 18:15-18, 25-27)

66Petro alipokuwa bado yuko chini kwenye ua wa jumba la kifalme, tazama akaja mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu. 67Alipomwona Petro akiota moto, akamtazama sana, akamwambia,

“Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

68Lakini Petro akakana, akasema, “Sijui wala sielewi unalosema.” Naye akaondoka kuelekea kwenye njia ya kuingilia.

69Yule mtumishi wa kike alipomwona mahali pale, akawaambia tena wale waliokuwa wamesimama hapo, “Huyu mtu ni mmoja wao.” 70Lakini Petro akakana tena.

Baada ya muda kidogo wale waliokuwa wamesimama hapo karibu na Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya!”
71Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui huyu mtu mnayesema habari zake!”

72Papo hapo jogoo akawika mara ya pili. Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alikuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Akavunjika moyo, akalia sana.
Copyright information for SwhNeno