‏ Mark 2:1-12

Yesu Amponya Mtu Aliyepooza

(Mathayo 9:1-8; Luka 5:17-26)

1Baada ya siku kadhaa Yesu alirudi Kapernaumu, watu wakasikia kwamba amerudi nyumbani. 2Hivyo watu wengi wakakusanyika kiasi kwamba hapakubaki nafasi yoyote hata mlangoni! Naye akawahubiria Neno. 3Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Yesu mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne. 4Kwa kuwa walikuwa hawawezi kumfikisha kwa Yesu kwa ajili ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa mahali pale alipokuwa Yesu, wakamshusha yule aliyepooza kwa kitanda alichokuwa amelalia. 5Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”

6Basi baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wameketi huko wakawaza mioyoni mwao, 7“Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”

8Mara moja Yesu akatambua rohoni mwake kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu? 9Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue mkeka wako, uende’? 10Lakini ili mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Yesu akamwambia yule aliyepooza, 11“Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” 12Yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama, akachukua mkeka wake, akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”
Copyright information for SwhNeno