Mark 5:21-43
Mwanamke Aponywa
(Mathayo 9:18-26; Luka 8:40-56)
21Yesu alipokwisha kuvuka tena na kufika ngʼambo, umati mkubwa wa watu ukamzunguka yeye akiwa hapo kando ya bahari. 22Kisha mmoja wa viongozi wa sinagogi aliyeitwa Yairo akafika pale. Naye alipomwona Yesu, akapiga magoti miguuni pake, 23akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali nakusihi, njoo uweke mikono yako juu yake ili apate kupona, naye atakuwa hai.” 24Hivyo Yesu akaenda pamoja naye. Umati mkubwa wa watu ukamfuata, nao watu wakawa wanamsonga. 25Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. 26Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi, na kutumia kila kitu alichokuwa nacho. Lakini badala ya kupona, hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27Alikuwa amesikia habari za Yesu, naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake, 28kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikiweza kuligusa vazi lake tu, nitaponywa.” 29Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa. 30Ghafula Yesu akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akaugeukia ule umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyegusa mavazi yangu?” 31Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi umati wa watu unavyokusonga. Wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ” 32Lakini Yesu akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa. 33Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. 34Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”Yesu Amfufua Binti Yairo
35Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo. Wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?” 36Aliposikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.” 37Hakumruhusu mtu mwingine yeyote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo. 38Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa. 39Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa, bali amelala tu.” 40Wale watu wakamcheka kwa dharau. Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto, pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao. Wakaingia ndani mpaka pale alipokuwa yule mtoto. 41Akamshika mtoto mkono, akamwambia, “Talitha koum!” ▼▼Talitha koum ni lugha ya Kiaramu.
(maana yake ni, “Msichana, nakuambia: amka!”) 42Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili). Walipoona haya, wakastaajabu sana. 43Yesu akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu yeyote jambo hilo, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.
Copyright information for
SwhNeno