‏ Mark 6:30-44

Yesu Awalisha Wanaume 5,000

(Mathayo 14:13-21; Luka 9:10-17; Yohana 6:1-14)

30Wale mitume wakakusanyika kwa Yesu na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. 31Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.”

32Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu. 33Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika. 34Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.

35Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimekwenda sana. 36Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula.”

37Lakini Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”

Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari 200
Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja; hivyo dinari 200 ni sawa na mshahara wa siku 200.
ili tuwape watu hawa wale?”

38Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.”

Walipokwisha kujua wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”

39Kisha Yesu akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani, 40nao wakaketi kwenye makundi ya watu mia mia na wengine hamsini hamsini. 41Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili. 42Watu wote wakala, wakashiba. 43Nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. 44Idadi ya wanaume waliokula walikuwa 5,000.
Copyright information for SwhNeno