‏ Mark 8:1-10

Yesu Alisha Wanaume 4,000

(Mathayo 15:32-39)

1Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia, 2“Ninauhurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula. 3Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.”

4Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?”

5Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?”

Wakajibu, “Tuna mikate saba.”

6Akawaambia watu waketi chini. Akiisha kuichukua mikate saba na kushukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo. 7Walikuwa pia na visamaki vichache, Yesu akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu. 8Wale watu walikula na kutosheka. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. 9Watu waliokula walikuwa wapata 4,000. Akiisha kuwaaga, 10aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha.
Copyright information for SwhNeno