‏ Matthew 19:1-12

Yesu Afundisha Kuhusu Talaka

(Marko 10:1-12)

1Yesu alipomaliza kusema maneno haya, aliondoka Galilaya, akaenda sehemu za Uyahudi, ngʼambo ya Mto Yordani. 2Umati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akawaponya huko.

3Baadhi ya Mafarisayo wakamjia ili kumjaribu, wakamuuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yoyote?”

4Akawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mwanaume na mwanamke, 5naye akasema, ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’? 6Hivyo si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

7Wakamuuliza, “Kwa nini basi Mose aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?”

8Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo. 9Mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.”

10Wanafunzi wake wakamwambia, “Kama hali ndiyo hii kati ya mume na mke, ni afadhali mtu asioe!”

11Yesu akawaambia, “Si watu wote wanaoweza kupokea neno hili, isipokuwa wale tu waliojaliwa na Mungu. 12Kwa maana wengine ni matowashi kwa sababu wamezaliwa hivyo; wengine wamefanywa matowashi na wanadamu; na wengine wamejifanya matowashi kwa ajili ya Ufalme wa Mbinguni. Yeye awezaye kulipokea neno hili na alipokee.”
Copyright information for SwhNeno