Matthew 19:16-30
Kijana Tajiri
(Marko 10:17-31; Luka 18:18-30)
16Mtu mmoja akamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?” 17Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.” 18Yule mtu akamuuliza, “Amri zipi?” Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, 19waheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.” 20Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?” 21Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” 22Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.Hatari Za Utajiri
23Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. 24Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.” 25Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?” 26Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.” 27Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, sisi tumeacha kila kitu na kukufuata! Tutapata nini basi?” 28Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, Mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti chake kitukufu cha enzi, ninyi mlionifuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29Kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu zake wa kiume au wa kike, baba au mama, watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo, na ataurithi uzima wa milele. 30Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.
Copyright information for
SwhNeno