‏ Matthew 22:1-10

Mfano Wa Karamu Ya Arusi

(Luka 14:15-24)

1Yesu akasema nao tena kwa mifano, akawaambia, 2“Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. 3Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja.

4 “Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba nimeandaa chakula. Nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono, karamu iko tayari. Karibuni kwa karamu ya arusi.’

5 “Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake. 6Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake, wakawatesa na kuwaua. 7Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto.

8 “Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja. 9Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni yeyote mtakayemwona.’ 10Wale watumishi wakaenda barabarani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni.
Copyright information for SwhNeno