‏ Matthew 26:57-75

Yesu Mbele Ya Kuhani Mkuu

(Marko 14:53-65; Luka 22:54-71; Yohana 18:13-24)

57Wale waliokuwa wamemkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, kuhani mkuu, mahali ambapo walimu wa sheria pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika. 58Lakini Petro akamfuata kwa mbali hadi uani kwa kuhani mkuu. Akaingia ndani, akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia.

59Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. 60Lakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza.

Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo
61na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”

62Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” 63Lakini Yesu akakaa kimya.

Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Kristo,
Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
Mwana wa Mungu.”

64Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

65Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia hayo makufuru. 66Uamuzi wenu ni gani?”

Wakajibu, “Anastahili kufa.”

67Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi 68na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?”

Petro Amkana Bwana Yesu

(Marko 14:66-72; Luka 22:56-62; Yohana 18:15-18, 25-27)

69Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mtumishi mmoja wa kike akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.”

70Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.”

71Alipotoka nje kufika kwenye lango, mtumishi mwingine wa kike alimwona, akawaambia watu waliokuwepo, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

72Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!”

73Baada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.”

74Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!”

Papo hapo jogoo akawika.
75Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alilokuwa amesema: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.
Copyright information for SwhNeno