Matthew 27:45-56
Kifo Cha Yesu
(Marko 15:33-41; Luka 23:44-49; Yohana 19:28-30)
45Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote. 46Ilipofika saa tisa, Yesu akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”) 47Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Eliya.” 48Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe. 49Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.” 50Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake. 51Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. 52Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa. 53Wakatoka makaburini, na baada ya Yesu kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi. 54Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa, wakasema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!” 55Walikuwako wanawake huko wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake. 56Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo na Yosefu, na mama yao wana wa Zebedayo.
Copyright information for
SwhNeno