Matthew 5:38-48
Kuhusu Kulipiza Kisasi
(Luka 6:29-30)
38 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ 39Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia. 40Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. 41Kama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. 42Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.Upendo Kwa Adui
(Luka 6:27-28, 32-36)
43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? 48Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
Copyright information for
SwhNeno