‏ Matthew 8:5-13

Yesu Amponya Mtumishi Wa Jemadari

(Luka 7:1-10)

5Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada, 6akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”

7Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”

8Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. 9Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”

10Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. 11Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni. 12Lakini warithi wa Ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwako kilio na kusaga meno.”

13Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona saa ile ile.
Copyright information for SwhNeno