‏ Numbers 20:1-13

Maji Kutoka Kwenye Mwamba

(Kutoka 17:1-7)

1Katika mwezi wa kwanza jumuiya yote ya Kiisraeli ilifika kwenye Jangwa la Sini, nao wakakaa Kadeshi. Miriamu akafa huko na kuzikwa.

2Mahali hapo hapakuwa na maji kwa ajili ya jumuiya hiyo, nao wakakusanyika ili kumpinga Mose na Aroni. 3Watu wakagombana na Mose, na kusema, “Laiti tungelikufa wakati ndugu zetu walipoanguka na kufa mbele za Bwana! 4Kwa nini mmeileta jumuiya ya Bwana kwenye jangwa hili, ili tufe humu, sisi na mifugo yetu? 5Kwa nini mmetupandisha kutoka Misri mpaka mahali hapa pa kutisha? Hapa hakuna nafaka wala tini, zabibu au makomamanga. Wala hapa hakuna maji ya kunywa!”

6Mose na Aroni wakaondoka pale kwenye kusanyiko mpaka kwenye mlango wa Hema la Kukutania na kuanguka kifudifudi, nao utukufu wa Bwana ukawatokea. 7Bwana akamwambia Mose, 8“Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Aroni mkusanye kusanyiko pamoja. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.”

9Kwa hiyo Mose akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele za Bwana kama alivyomwagiza. 10Mose na Aroni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Mose akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?” 11Ndipo Mose akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa.

12Lakini Bwana akamwambia Mose na Aroni, “Kwa sababu hamkuniamini mimi kiasi cha kuniheshimu kama mtakatifu machoni pa Waisraeli, hamtaiingiza jumuiya hii katika nchi ninayowapa.”

13Haya yalikuwa maji ya Meriba,
Meriba maana yake Kugombana.
mahali pale ambapo Waisraeli waligombana na Bwana, naye akajionyesha mwenyewe huko kuwa mtakatifu katikati yao.
Copyright information for SwhNeno