‏ Numbers 27:12-23

Yoshua Kuchukua Nafasi Ya Mose

(Kumbukumbu 31:1-8)

12Kisha Bwana akamwambia Mose, “Panda juu ya mlima huu katika kilele cha Abarimu uione nchi ambayo nimewapa Waisraeli. 13Baada ya kuiona, wewe pia utakusanywa pamoja na watu wako kama ndugu yako Aroni alivyokusanywa, 14kwa kuwa jumuiya ilipoasi amri yangu kwenye maji katika Jangwa la Sini, wakati jumuiya ilipogombana nami, nyote wawili mliacha kuitii amri yangu ya kuniheshimu kama mtakatifu mbele ya macho yao.” (Haya yalikuwa maji ya Meriba huko Kadeshi, katika Jangwa la Sini.)

15Mose akamwambia Bwana, 16Bwana, Mungu wa roho zote za wanadamu, na amteue mtu juu ya jumuiya hii 17ili atoke na kuingia mbele yao, atakayewaongoza katika kutoka kwao na kuingia kwao, ili watu wa Bwana wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji.”

18Kwa hiyo Bwana akamwambia Mose, “Mchukue Yoshua mwana wa Nuni, mtu ambaye Roho yuko ndani yake, uweke mkono juu yake. 19Msimamishe mbele ya kuhani Eleazari pamoja na kusanyiko lote, umpe maagizo mbele yao. 20Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli ipate kumtii. 21Atasimama mbele ya kuhani Eleazari, ambaye atapokea maamuzi kwa ajili yake, kwa kuuliza mbele za Bwana kwa ile Urimu.
Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha.
Kwa amri yake, yeye na jumuiya yote ya Waisraeli watatoka, na kwa amri yake, wataingia.”

22Mose akafanya kama Bwana alivyomwagiza. Akamtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na kusanyiko lote. 23Kisha akaweka mikono yake juu ya kichwa cha Yoshua na kumpa maagizo, kama vile Bwana alivyoelekeza kupitia kwa Mose.
Copyright information for SwhNeno