‏ Numbers 9:15-23

Wingu La Moto Juu Ya Maskani

(Kutoka 40:34-38)

15Katika siku hiyo ambayo Maskani, Hema la Ushuhuda, iliposimamishwa, wingu liliifunika. Kuanzia jioni mpaka asubuhi wingu lililokuwa juu ya Maskani lilionekana kama moto. 16Hivyo ndivyo lilivyoendelea kuwa; wingu liliifunika wakati wa mchana, na usiku lilionekana kama moto. 17Wakati wowote wingu lilipoinuka kutoka juu ya Hema, nao Waisraeli waliondoka; mahali popote wingu liliposimama, Waisraeli walipiga kambi. 18Kwa amri ya Bwana Waisraeli waliondoka, na kwa amri yake walipiga kambi. Kwa muda wote wingu liliposimama juu ya Maskani, Waisraeli walibaki wamepiga kambi.

19Wakati wingu lilipobaki juu ya Maskani kwa muda mrefu, Waisraeli walitii amri ya Bwana nao hawakuondoka. 20Wakati mwingine wingu lilikuwa juu ya Maskani kwa siku chache tu; kwa amri ya Bwana wangelipiga kambi na kisha kwa amri yake wangeliondoka. 21Wakati mwingine wingu lilikuwepo kuanzia jioni mpaka asubuhi tu, na lilipoinuka asubuhi, nao waliondoka. Ikiwa ni mchana au usiku, wakati wowote wingu lilipoinuka, waliondoka. 22Ikiwa wingu lilikaa juu ya Maskani kwa siku mbili au mwezi au mwaka, Waisraeli wangebaki wamepiga kambi na hawakuondoka; lakini lilipoinuka, wangeondoka.

23Kwa amri ya Bwana walipiga kambi, na kwa amri ya Bwana waliondoka. Walitii amri ya Bwana, kufuatana na agizo lake kupitia Mose.
Copyright information for SwhNeno