‏ Psalms 105:1-15

Uaminifu Wa Mungu Kwa Israeli

(1 Nyakati 16:8-22)

1Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake,
wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.
2Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa,
waambieni matendo yake yote ya ajabu.
3Lishangilieni jina lake takatifu,
mioyo ya wale wamtafutao Bwana na ifurahi.
4Mtafuteni Bwana na nguvu zake,
utafuteni uso wake siku zote.

5Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya,
miujiza yake na hukumu alizozitamka,
6enyi wazao wa Abrahamu mtumishi wake,
enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
7Yeye ndiye Bwana Mungu wetu,
hukumu zake zimo duniani pote.

8Hulikumbuka agano lake milele,
neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
9agano alilolifanya na Abrahamu,
kiapo alichomwapia Isaki.
10Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri,
kwa Israeli liwe agano la milele:
11“Nitakupa wewe nchi ya Kanaani
kuwa sehemu utakayoirithi.”

12Walipokuwa wachache kwa idadi,
wachache sana na wageni ndani yake,
13walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine,
kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
14Hakuruhusu mtu yeyote awaonee;
kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema:
15“Msiwaguse niliowatia mafuta;
msiwadhuru manabii wangu.”
Copyright information for SwhNeno