1 Corinthians 1

Salamu

1Paulo, aliyeitwa kwa mapenzi ya Mungu kuwa mtume wa Yesu Kristo na Sosthene ndugu yetu.

2Kwa Kanisa la Mungu lililoko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa kuwa watakatifu, pamoja na wale wote ambao kila mahali wanaliitia Jina la Kristo Yesu Bwana wetu, aliye Bwana wao na wetu pia:

3Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.

Shukrani

4Ninamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu kwa sababu ya neema yake mliyopewa katika Kristo Yesu. 5Kwa kuwa katika Kristo mmetajirishwa kwa kila hali, katika kusema kwenu na katika maarifa yenu yote, 6kwa sababu ushuhuda wetu kumhusu Yesu ulithibitishwa ndani yenu. 7Kwa hiyo hamkupungukiwa na karama yo yote ya kiroho wakati mnangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. 8Yeye atawafanya imara mpaka mwisho, ili msiwe na hatia siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. 9Mungu ni mwaminifu, ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Yesu Kristo, Bwana wetu.

Mgawanyiko Ndani Ya Kanisa

10Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano katikati yenu na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi. 11Kwa maana ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi katikati yenu. 12Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa
1:12 Yaani Petro
”; na mwingine, “Mimi ni wa Kristo.”

13Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulibishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? 14Namshukuru Mungu kwamba sikumbatiza mtu ye yote miongoni mwenu isipokuwa Krispo na Gayo. 15Kwa hiyo hakuna mtu ye yote miongoni mwenu anayeweza kusema kwamba alibatizwa kwa Jina langu. 16(Naam, niliwabatiza pia watu wa nyumbani mwa Stefana. Lakini zaidi ya hao sijui kama nilimbatiza mtu mwingine ye yote.) 17Kwa maana Kristo hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili na nifanye hivyo si kwa kutumia maneno ya hekima ya kibinadamu ya kushawishi, ili msalaba wa Kristo usije ukakosa nguvu yake.

Kristo Hekima Na Nguvu Ya Mungu

18Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. 19Kwa maana imeandikwa: “Nitaiharibu hekima ya wenye hekima,
na kuzibatilisha akili za wenye akili.”20Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu? 21Kwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale waaminio kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. 22Wayahudi wanataka miujiza na Wayunani wanatafuta hekima, 23lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulibiwa, ambaye kwa Wayahudi ni kitu cha kukwaza na kwa Wayunani ni upuzi. 24Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi pia Wayunani, Kristo ni nguvu na hekima ya Mungu. 25Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.

26Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na nguvu, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili aviaibishe vyenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili aviaibishe vyenye nguvu. 28Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29ili mtu ye yote asijisifu mbele za Mungu. 30Mungu ndiye chanzo cha uzima wenu katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu na haki na utakaso na ukombozi, 31ili kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

Copyright information for Neno