1 Corinthians 16

Changizo Kwa Ajili Ya Watakatifu

1 aBasi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. 2 bSiku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango. 3 cKwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu. 4 dKama ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.

Mahitaji Binafsi

5 eBaada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia. 6 fHuenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendapo. 7 gKwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu; natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana akipenda. 8 hLakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste, 9 ikwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi wanaonipinga.

10 jIkiwa Timotheo atakuja kwenu, hakikisheni kwamba hana hofu yoyote akiwa nanyi, kwa sababu anafanya kazi ya Bwana, kama mimi nifanyavyo. 11 kBasi asiwepo mtu atakayekataa kumpokea. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunijia tena. Namtarajia pamoja na ndugu.

12 lBasi kwa habari za ndugu yetu Apolo, nimemsihi kwa bidii aje kwenu pamoja na hao ndugu. Ingawa alikuwa hapendi kabisa kuja sasa, lakini atakuja apatapo nafasi.

Maneno Ya Mwisho

13 mKesheni, simameni imara katika imani, fanyeni kiume, kuweni mashujaa kuweni hodari. 14 nFanyeni kila kitu katika upendo.

15 oNinyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio waliokuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi, 16 pmjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii. 17 qNilifurahi wakati Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu. 18 rKwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa.

Salamu Za Mwisho

19 sMakanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Prisila,
Prisila kwa Kiyunani ni Priska, hivyo tafsiri nyingine zimemuita Priska.
pamoja na kanisa lililoko nyumbani kwao wanawasalimu sana katika Bwana.
20 uNdugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.

21 vMimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe.

22 wKama mtu yeyote hampendi Bwana Yesu Kristo, na alaaniwe. Bwana wetu, njoo.
Kwa Kiaramu ni Marana tha.


23 yNeema ya Bwana Yesu iwe nanyi.

24Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu. Amen.

Copyright information for SwhNEN