1 Corinthians 3

Kuhusu Mgawanyiko Katika Kanisa

1Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwilini, kama watoto wachanga katika Kristo. 2Naliwanywesha maziwa, wala si chakula kigumu, kwa kuwa hamkuwa tayari kwa hicho chakula kigumu. Naam, hata sasa hamkiwezi. 3Kwa maana ninyi bado ni watu wa mwilini. Kwa kuwa bado kuna wivu na magombano miongoni mwenu, je, ninyi si watu wa mwilini, nanyi mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? 4Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” mwingine, “Mimi ni wa Apolo,” je, ninyi si wanadamu wa kawaida?

5Kwani, Apolo ni nani? Naye Paulo ni nani? Ni watumishi tu ambao kwa kupitia wao mliamini. 6Mimi nilipanda mbegu, Apolo akatia maji, lakini Mungu ndiye aliyekuza. 7Hivyo mwenye kupanda mbegu na mwenye kutia maji si kitu, bali Mungu peke yake ndiye akuzaye. 8Apandaye mbegu ni sawa na yule atiaye maji. Kila mmoja atalipwa kulingana na kazi yake. 9Sisi ni watenda kazi pamoja na Mungu, ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.

10Kwa neema Mungu aliyonipa, niliweka msingi kama mjenzi stadi na mtu mwingine anajenga juu ya huo msingi. Lakini kila mmoja inampasa awe mwangalifu jinsi anavyojenga juu yake. 11Kwa maana hakuna mtu ye yote awezaye kuweka msingi mwingine wo wote isipokuwa ule uliokwisha kuwekwa, ambao ni Yesu Kristo. 12Kama mtu ye yote akijenga juu ya msingi huu kwa kutumia dhahabu, fedha, mawe ya thamani, miti, majani au nyasi, 13kazi yake itaonekana kuwa ikoje, kwa kuwa siku ile itaidhihirisha kazi yake. Itadhihirishwa kwa moto, nao moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu. 14Kama kile alichojenga kitabaki, atapokea thawabu. 15Kama kazi ya mtu itateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini kama mtu aliyenusurika kwenye moto.

16Je, hamjui ya kwamba ninyi ni Hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17Kama mtu ye yote akiliharibu Hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza mtu huyo, Kwa maana Hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.

18Msijidanganye. Kama mtu ye yote miongoni mwenu akidhani kuwa ana hekima kwa viwango vya dunia hii, inampasa awe mjinga ili apate kuwa na hekima. 19Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuzi mbele za Mungu. Kama ilivyoandikwa: “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao,” 20Tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni ubatili.” 21Hivyo basi, mtu asijivune kuhusu wanadamu! Kwa kuwa vitu vyote ni vyenu, 22ikiwa ni Paulo au Apolo au Kefa
3:22 Yaani Petro
au dunia au uzima au mauti, au wakati uliopo au wakati ujao, haya yote ni yenu
23na ninyi ni wa Kristo, naye Kristo ni wa Mungu.

Copyright information for Neno