1 Corinthians 8

Chakula Kilichotolewa Sadaka Kwa Sanamu

Sasa kuhusu chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sisi sote tuna ujuzi.” Lakini ujuzi hujivuna, bali upendo hujenga. Mtu ye yote anayedhani kwamba anajua kitu, hajui kama impasavyo kujua. Lakini mtu ampendaye Mungu, hujulikana naye.

Hivyo basi, kuhusu kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sanamu si kitu cho chote kabisa duniani na kwamba kuna Mungu mmoja tu.” Kwa maana hata kama wapo hao wanaoitwa “miungu” kama ni mbinguni au duniani (kama ilivyo kweli wapo “miungu” wengi na “mabwana” wengi). Lakini kwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa yeye vitu vyote vimekuwepo na kwa yeye sisi tunaishi.

Lakini si wote wanaojua jambo hili. Baadhi ya watu bado wamezoea kufikiria kuwa sanamu ni halisi hivyo wanapokula chakula kama hicho wanadhani kimetolewa sadaka kwa sanamu na kwa kuwa dhamiri zao ni dhaifu, kinatiwa unajisi. Lakini chakula hakituleti karibu na Mungu wala hatupotezi cho chote tusipokula, wala hatuongezi cho chote kama tukila.

Lakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu katika imani. 10 Kwa maana kama mtu ye yote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu? 11 Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu. 12 Mnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Kristo. 13 Kwa hiyo, kama kile ninachokula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe muda nchi idumupo, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.

Copyright information for Neno