1 John 2

Kristo Mwombezi Wetu

1Watoto wangu wapendwa, nawaandikieni haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu ye yote akitenda dhambi, tunaye mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo mwenye haki. 2Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

3Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua kama tunazishika amri zake. 4Mtu ye yote asemaye kuwa, “Ninamjua” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli. 5Lakini kama mtu ye yote analitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake. 6Ye yote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.

Amri Mpya

7Wapenzi, siwaandikii ninyi amri mpya bali ile ya zamani, ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ya zamani ni lile neno mlilosikia. 8Lakini ninawaandikia amri mpya, yaani, lile neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu, kwa sababu giza linapita na ile nuru ya kweli tayari inang'aa.

9Ye yote anayesema yumo nuruni lakini anamchukia ndugu yake bado yuko gizani. 10Yeye ampendaye ndugu yake anakaa nuruni, wala hakuna kitu cho chote ndani yake cha kumkwaza. 11Lakini ye yote amchukiaye ndugu yake, yuko gizani na anaenenda gizani, wala hajui anakokwenda, kwa sababu giza limempofusha macho. 12Nawaandikia ninyi, watoto wadogo,
kwa sababu dhambi zenu
zimesamehewa kwa ajili ya Jina lake.
13Nawaandikia ninyi, akina baba,
kwa sababu mmemjua
yeye aliye tangu mwanzo.
Nawaandikia ninyi vijana
kwa sababu mmemshinda yule mwovu.
Nawaandikia ninyi watoto wadogo,
kwa sababu mmemjua Baba.
14Nawaandikia ninyi akina baba,
kwa sababu mmemjua
yeye aliye tangu mwanzo.
Nawaandikia ninyi vijana,
kwa sababu mna nguvu,
na neno la Mungu linakaa ndani yenu,
nanyi mmemshinda yule mwovu.


Msiupende Ulimwengu

15Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyoko ulimwenguni. Kama mtu ye yote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake. 16Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima: havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu. 17Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.

Onyo Dhidi Ya Wapinga Kristo

18Watoto wadogo, huu ni wakati wa mwisho! Kama mlivyosikia kwamba mpinga Kristo anakuja, hivyo basi wapinga Kristo wengi wamekwisha kuja. Kutokana na hili twajua kwamba huu ni wakati wa mwisho. 19Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu hasa. Kwa maana kama wangelikuwa wa kwetu, wangelikaa pamoja nasi, lakini kutoka kwao kulionyesha kwamba hakuna hata mmoja wao aliyekuwa wa kwetu.

20Lakini ninyi mmetiwa mafuta na yeye Aliye Mtakatifu, nanyi nyote mnaijua kweli. 21Siwaandikii kwa sababu hamuijui kweli, bali kwa sababu mnaijua, nanyi mnajua hakuna uongo utokao katika kweli. 22Je, mwongo ni nani? Mwongo ni mtu yule asemaye kwamba Yesu si Kristo. Mtu wa namna hiyo ndiye mpinga Kristo, yaani, yeye humkana Baba na Mwana. 23Hakuna ye yote amkanaye Mwana aliye na Baba. Ye yote anayemkubali Mwana anaye na Baba pia.

24Hakikisheni kwamba lile mlilosikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu. Kama lile mlilosikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana na ndani ya Baba. 25Hii ndiyo ahadi yake kwetu, yaani, uzima wa milele.

26Ninawaandikia mambo haya kuhusu wale watu ambao wanajaribu kuwapotosha. 27Kwa habari yenu ninyi, upako ule mlioupata kutoka kwake unakaa ndani yenu, wala ninyi hamna haja ya mtu ye yote kuwafundisha. Lakini kama vile upako wake unavyowafundisha kuhusu mambo yote nayo ni kweli wala si uongo, basi kama ulivyowafundisha kaeni ndani yake.

Watoto Wa Mungu

28Sasa basi, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili atakapofunuliwa, tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake wakati wa kuja kwake.

29Kama mkijua kuwa yeye ni mwenye haki, mwajua kwamba kila atendaye haki amezaliwa na yeye.

Copyright information for Neno