1 Kings 3

Solomoni Anaomba Hekima

Solomoni akafanya urafiki na Mfalme Farao wa Misri na kumwoa binti yake. Akamleta huyo binti katika Mji wa Daudi mpaka alipomaliza kujenga jumba lake la kifalme na Hekalu la BWANA, pamoja na ukuta kuzunguka Yerusalemu. Hata hivyo, watu bado walikuwa wakitoa dhabihu huko kwenye vilima, kwa sababu Hekalu lilikuwa bado halijajengwa kwa ajili ya Jina la BWANA. Solomoni akaonyesha upendo wake kwa BWANA kwa kuenenda sawasawa na amri za Daudi baba yake, ila yeye alitoa dhabihu na kufukiza uvumba huko mahali pa juu.

Mfalme akaenda Gibeoni kutoa dhabihu, kwa maana ndipo palipokuwa mahali maarufu zaidi, naye Solomoni akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu ya hiyo madhabahu. BWANA akamtokea Solomoni huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lo lote utakalo nikupe.”

Solomoni akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako baba yangu Daudi fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu na umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme kama ilivyo leo.

“Sasa, Ee BWANA Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme baada ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu. Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua. Taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao. Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi?”

10 Bwana akapendezwa kwamba Solomoni ameliomba jambo hili. 11 Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba ufahamu katika kutoa haki, 12 nitafanya lile uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwepo mtu mwingine kama wewe wala kamwe hatakuwapo baada yako. 13 Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba, yaani utajiri na heshima, ili kwamba maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme. 14 Nawe kama ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu kama baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.” 15 Ndipo Solomoni akaamka, akatambua kuwa alikuwa katika ndoto.

Akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya Sanduku la Agano la BWANA, naye akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha akawafanyia watumishi wake wote karamu.

Utawala Wa Hekima

16 Basi wanawake wawili makahaba walikuja kwa mfalme na kusimama mbele yake. 17 Mmojawapo akasema, “Bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunaishi kwenye nyumba moja. Nilikuwa nimezaa alipokuwa pamoja nami. 18 Siku ya tatu baada ya mtoto wangu kuzaliwa, mwanamke huyu pia naye akazaa mtoto. Tulikuwa peke yetu, hapakuwa na mtu mwingine ye yote katika nyumba isipokuwa sisi wawili.

19 “Wakati wa usiku mwana wa huyu mwanamke akafa kwa sababu alimlalia. 20 Hivyo akaondoka katikati ya usiku na kumchukua mwanangu kutoka ubavuni pangu wakati mimi mtumishi wako nilipokuwa nimelala. Akamweka kifuani mwake na kumweka mwanawe aliyekufa kifuani mwangu. 21 Asubuhi yake, nikaamka ili kumnyonyesha mwanangu, naye alikuwa amekufa! Lakini nilipomwangalia sana katika nuru ya asubuhi, niliona kuwa hakuwa yule mwana niliyekuwa nimemzaa.”

22 Huyo mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Mwana aliye hai ndiye wangu, aliyekufa ni wako.”

Lakini yule wa kwanza akasisitiza, “Hapana! Mwana aliyekufa ni wako, aliye hai ni wangu.” Hivi ndivyo walivyobishana mbele ya mfalme.

23 Mfalme akasema, “Huyu anasema, ‘Mwanangu ndiye aliye hai, na aliyekufa ndiye mwanao,’ maadamu yule anasema, ‘Hapana! Aliyekufa ni wako, na aliye hai ni wangu.’ ”

24 Kisha mfalme akasema, “Nileteeni upanga.” Basi wakamletea mfalme upanga. 25 Ndipo mfalme akatoa amri: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili; mpe huyu nusu na mwingine nusu.”

26 Mwanamke ambaye mwanawe alikuwa hai akajawa na huruma kwa ajili ya mwanawe na kumwambia mfalme, “Tafadhali, bwana wangu, mpe yeye mtoto aliye hai! Usimue!”

Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Mkate vipande viwili. Asiwe wangu au wake!”

27 Kisha mfalme akatoa uamuzi wake: “Mpeni mama wa kwanza mtoto aliye hai. Msimue; ndiye mama yake.”

28 Wakati Israeli yote iliposikia hukumu aliyotoa mfalme, wakamwogopa mfalme, kwa sababu waliona kuwa alikuwa na hekima kutoka kwa Mungu kwa kutoa haki.

Copyright information for Neno