1 Samuel 23

Daudi Aokoa Keila

1Daudi alipoambiwa kuwa, “Tazama, Wafilisti wanapigana dhidi ya Keila nao wanapokonya nafaka katika sakafu za kupuria,” 2akauliza kwa BWANA, akisema, “Je, niende na kuwashambulia hawa Wafilisti?”

BWANA akamjibu, “Nenda, washambulie Wafilisti na uiokoe Keila.”

3Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Hapa Yuda kwenyewe tunaogopa. Si zaidi sana, kama tukienda Keila dhidi ya majeshi ya Wafilisti!”

4Daudi akauliza kwa BWANA tena, naye BWANA akamjibu akamwambia, “Shuka uende Keila, kwa kuwa nitawatia Wafilisti mkononi mwako.” 5Basi Daudi na watu wake wakaenda Keila, wakapigana na Wafilisti na kutwaa wanyama wao wa kutosha. Daudi akawatia hasara kubwa Wafilisti na kuwaokoa watu wa Keila. 6(Basi Abiathari mwana wa Ahimeleki alikuwa ameleta kisibau alipokimbilia kwa Daudi huko Keila.)

Sauli Anamfuata Daudi

7Sauli akaambiwa kwamba Daudi alikuwa amekwenda Keila, naye akasema, “Mungu amemtia mkononi mwangu, kwa kuwa Daudi amejifunga mwenyewe kwa kuingia kwenye mji wenye malango na makomeo.” 8Naye Sauli akayaita majeshi yake yote yaende vitani, kuishukia Keila ili kumzingira Daudi na watu wake kwa jeshi.

9Daudi alipojua kuwa Sauli alikuwa ana hila dhidi yake, akamwambia Abiathari kuhani, “Leta kile kisibau.” 10Daudi akasema, “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mtumishi wako amesikia kwa hakika kwamba Sauli anapanga kuja Keila na kuangamiza mji kwa ajili yangu. 11Je, watu wa Keila watanisalimisha kwake? Je, Sauli atatelemka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mwambie mtumishi wako.”

Naye BWANA akasema, “Ndiyo, atashuka.”

12Daudi akauliza tena, “Je watu wa Keila watanisalimisha mimi pamoja na watu wangu kwa Sauli?”

Naye BWANA akasema, “Ndiyo, watafanya hivyo.”

13Basi Daudi na watu wake, wapatao 600, wakaondoka Keila wakawa wanakwenda sehemu moja hadi nyingine. Sauli alipoambiwa Daudi ametoroka kutoka Keila, hakwenda huko.

14Daudi akakaa katika ngome za jangwani na katika vilima vya Jangwa la Zifu. Siku baada ya siku aliendelea kumsaka, lakini Mungu hakumtia Daudi mikononi mwake.

15Daudi alipokuwa huko Horeshi katika Jangwa la Zifu, akajua kuwa Sauli alikuwa amekuja ili amuue. 16Naye Yonathani mwana wa Sauli akamwendea Daudi huko Horeshi na kumtia moyo kusimama imara katika imani yake kwa Mungu. 17Akamwambia, “Usiogope, Daudi; baba yangu Sauli hatakutia mkononi mwake. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, nami nitakuwa wa pili wako. Hata baba yangu Sauli anajua hili.” 18Wote wawili wakaweka agano mbele za BWANA. Kisha Yonathani akaenda zake nyumbani, lakini Daudi akabaki Horeshi.

19Basi Wazifu wakakwea kwa Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu katika ngome huko Horeshi, katika kilima cha Hakila, kusini ya Yeshimoni? 20Sasa, Ee mfalme, utelemke wakati wo wote unapoona vyema kufanya hivyo, sisi tutawajibika kumkabidhi kwa mfalme.”

21Sauli akajibu, “BWANA awabariki kwa kunifikiria. 22Nendeni mkafanye maandalizi zaidi. Mkajue mahali ambapo Daudi huenda mara kwa mara na nani amepata kumwona huko. Wananiambia yeye ni mwerevu sana. 23Jueni kila mahali anapojificha mrudi na kunipa taarifa kamili. Kisha nitakwenda pamoja nanyi, kama atakuwa katika eneo hilo, nitamsaka miongoni mwa koo zote za Yuda.”

24Basi wakaondoka na kwenda mpaka Zifu wakimtangulia Sauli. Naye Daudi na watu wake walikuwa katika Jangwa la Maoni, katika Araba kusini ya Yeshimoni. 25Sauli na watu wake wakaanza msako, naye Daudi alipoelezwa hili, akatelemka mpaka mwambani na kukaa katika Jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hili, akaenda katika Jangwa la Maoni akimfuata Daudi.

26Sauli alikuwa akienda upande mmoja wa mlima, naye Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima, wakiharakisha kumkimbia Sauli. Wakati Sauli na majeshi yake walipokaribia kumkamata Daudi na watu wake, 27mjumbe alikuja kwa Sauli, akisema, “Njoo haraka! Wafilisti wanashambulia nchi.” 28Ndipo Sauli akarudi akaacha kumfuata Daudi na kwenda kukabiliana na Wafilisti. Ndiyo sababu wanaiita sehemu hii Sela-Hamahlekothi
23.28 Sela-Hamahlekothi maana yake Mwamba wa Kutengana
.
29Naye Daudi akakwea kutoka huko na kuishi katika ngome za En-Gedi.

Copyright information for Neno