1 Timothy 1

Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na ya Kristo Yesu tumaini letu.

Kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani:

Neema, rehema na amani kutoka kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.

Maonyo Dhidi Ya Walimu Wa Uongo

Kama nilivyokusihi kuendelea kubaki Efeso, wakati nilipokwenda Makedonia, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha zisizo na mwisho za majina ya vizazi ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Kimungu utokanao na imani. Kusudi la maagizo haya ni upendo, utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli. Watu wengine wamepotoka kutoka katika haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.

Tunajua kwamba sheria ni njema ikiwa inatumika kwa halali kama ilivyokusudiwa. Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru, kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji, 10 kwa wazinzi na wahanithi, wauza watu na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa cho chote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli, 11 ambayo yanakubaliana na Injili ya utukufu wa Mungu anayehimidiwa, ambayo mimi Paulo nimewekea amana.

Neema Ya Mungu Kwa Paulo

12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake. 13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri. Lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutokujua na kutokuamini kwangu. 14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.

15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote. 16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili kwamba katika mimi niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini wapate uzima wa milele. 17 Basi, Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.

18 Mwanangu Timotheo, ninakupa agizo hili, kwa kadiri ya maneno ya unabii yaliyosemwa kukuhusu, ili kwa kuyafuata upate kupigana vile vita vizuri, 19 ukiishikilia imani na dhamiri njema ambayo wengine wamevikataa na hivyo, wakaangamia kwa habari ya imani yao. 20 Miongoni mwao wako Himenayo na Aleksanda, ambao nimemkabidhi Shetani ili wafundishwe wasije wakakufuru.

Copyright information for Neno