1 Timothy 5

Maagizo Kuhusu Wajane, Wazee Na Watumwa

1Usimkemee mzee kwa ukali bali umuonye kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako, 2wanawake wazee uwatendee kama mama zako na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote.

3Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli. 4Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo, kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe ili wawarudishie wema ule wazazi wao waliowatendea, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu. 5Mwanamke ambaye ni mjane kweli kweli, yaani, yeye aliyebaki peke yake huweka tumaini lake kwa Mungu naye hudumu katika maombi usiku na mchana akimwomba Mungu ili amsaidie. 6Lakini mjane aishiye kwa anasa, amekufa, ingawa anaishi. 7Wape watu maagizo haya pia, ili asiwepo ye yote wa kulaumiwa. 8Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.

9Mjane ye yote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na ambaye alikuwa mke wa mume mmoja, 10awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna.

11Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena. 12Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza. 13Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema. 14Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu. 15Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani.

16Lakini kama mwanamke ye yote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kanisa, ili kanisa liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.

Wazee Wa Kanisa

17Wazee wa kanisa wanaoongoza shughuli za kanisa vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha. 18Kwa maana Maandiko husema, “Usimfunge ng'ombe kinywa apurapo nafaka,” tena, “Mfanyakazi anastahili mshahara wake.” 19Usiendekeze mashtaka dhidi ya mzee isipokuwa yawe yameletwa na mashahidi wawili au watatu. 20Wale wanaodumu katika dhambi uwakemee hadharani, ili wengine wapate kuogopa.

21Ninakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu na mbele za malaika wateule, shika maagizo haya pasipo ubaguzi wala upendeleo.

22Usiwe na haraka kumwekea mtu mikono wala usishiriki dhambi za watu wengine. Jilinde nafsi yako uwe safi.

23Acha kunywa maji peke yake, tumia divai kidogo kwa sababu ya tumbo lako na maumivu yako ya mara kwa mara.

24Dhambi za watu wengine ni dhahiri nazo zinawatangulia kwenda hukumuni na dhambi za watu wengine zinawafuata nyuma yao. 25Vivyo hivyo, matendo mema yako dhahiri, na hata yale ambayo si mema hayawezi kufichika.

Copyright information for Neno