1 Timothy 6

Watumwa

1Wale wote walio chini ya kongwa la utumwa inawapasa kuwahesabu mabwana zao kuwa wanastahili heshima yote, ili jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu. 2Wale watumwa ambao wana mabwana waaminio, haiwapasi kupunguza heshima yao kwa sababu wao ni ndugu, badala yake, wawatumikie hata vizuri zaidi, kwa sababu wale wanaonufaika na huduma yao ni waaminio, ambao ni wapenzi wao.

Mafundisho Ya Uongo Na Utajiri Wa Kweli

3Ikiwa mtu ye yote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, huyo amejivuna wala hajui kitu cho chote. 4Yeye ni mgonjwa aliyejaa tamaa ya mabishano na ugomvi ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya 5na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.

6Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu cho chote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka haraka huanguka kwenye majaribu na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu, zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

Vitu Vizuri Vya Imani

11Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole. 12Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi. 13Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai na mbele za Kristo Yesu ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri, 14uishike amri hii bila dosari wala lawama mpaka kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, 15ambaye Mungu atamleta kwa wakati wake mwenyewe, yeye ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana. 16Yeye peke yake hapatikani na mauti, ambaye anakaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa, ambaye hakuna mwanadamu aliyemwona wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye milele. Amen.

17Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

Maelekezo Ya Binafsi Na Maombi Ya Baraka

20Timotheo, linda kile kilichowekwa amana kwako. Epuka majadiliano yasiyo ya utauwa na mabishano ambayo kwa uongo huitwa elimu, 21ambayo wengine kwa kujidai kuwa nayo wameiacha imani.

Neema iwe nanyi. Amen.

Copyright information for Neno