2 Chronicles 23

Uasi Dhidi Ya Athalia

1Katika mwaka wa saba Yehoyada akaonyesha nguvu zake. Akafanya agano na majemadari wa vikosi vya mamia: Azaria mwana wa Yehoramu, Ishmaeli mwana wa Yehohanani, Azaria mwana wa Obedi, Maaseya mwana wa Adaya na Elishafati mwana wa Zikri. 2Wakazunguka katika Yuda yote na kukusanya Walawi na viongozi wa jamaa za Israeli kutoka katika miji yote. Walipofika Yerusalemu, 3kusanyiko lote likafanya agano na mfalme kwenye Hekalu la Mungu.

Yehoyada akawaambia, “Mwana wa mfalme atatawala, kama BWANA alivyoahidi kuhusu wazao wa Daudi.
4Basi hili ndilo liwapasalo kufanya: Theluthi ya makuhani wenu na Walawi ambao watakuwa kwenye zamu siku ya Sabato watalinda milangoni, 5theluthi watalinda jumba la kifalme, theluthi nyingine watalinda Lango la Msingi. Watu wengine wote itawapasa wawe ndani ya nyua za Hekalu la BWANA. 6Hakuna ruhusa mtu ye yote kuingia Hekaluni mwa BWANA isipokuwa makuhani na Walawi walioko kwenye zamu. Wao wanaweza kuingia kwa sababu ni watakatifu, lakini watu wengine wote itawapasa kuangalia kile kilichoamriwa na BWANA. 7Walawi watajipanga kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha zake mkononi. Mtu mwingine ye yote aingiaye Hekaluni lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme po pote aendapo.”

8Walawi na watu wote wa Yuda wakafanya vile vile kama Kuhani Yehoyada alivyoagiza. Kila mmoja akachukua watu wake, wale waliokuwa wakienda kwenye zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakitoka kwenye zamu, kwa sababu Kuhani Yehoyada hakuruhusu kikosi cho chote kiondoke. 9Kisha akawapa majemadari wa vikosi vya mamia mikuki na ngao kubwa na ndogo zilizokuwa mali ya Mfalme Daudi na ambazo zilikuwa ndani ya Hekalu la Mungu. 10Akawapanga walinzi kumzunguka mfalme, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi. Wakakaa kwenye mduara kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini wa Hekalu wakiizunguka madhabahu yote.

11Yehoyada na wanawe wakamtoa nje Yoashi mwana wa mfalme nao wakamvika taji wakampa nakala ya Agano na kumtangaza kuwa mfalme. Yehoyada na wanawe wakamtia mafuta, nao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”

12Athalia aliposikia kelele za watu wakikimbia na kumsifu mfalme, akawaendea watu katika Hekalu la BWANA. 13Athalia akaangalia, tazama alikuwepo mfalme akiwa amesimama karibu na nguzo yake kwenye ingilio. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa kando ya mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wanashangilia na kupiga tarumbeta na waimbaji wakiwa na vyombo vya uimbaji, walikuwa wakiongoza nyimbo za sifa. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kupiga kelele, akisema, “Uhaini! Uhaini!”

14Kuhani Yehoyada akawatoa nje majemadari wa vikosi vya mia, waliokuwa viongozi wa jeshi na kuwaambia: “Mtoeni nje kati ya safu na mkamwue kwa upanga ye yote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Msimwulie ndani ya Hekalu la BWANA.” 15Kwa hiyo wakamkamata alipofika kwenye ingilio la Lango la Farasi katika viwanja vya jumba la kifalme wakamwulia hapo.

16Kisha Yehoyada akafanya agano kwamba yeye na watu wote pamoja na mfalme watakuwa watu wa BWANA. 17Kisha watu wote wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu pamoja na sanamu na kumwua Matani kuhani wa Baali mbele ya hizo madhabahu.

18Kisha Kuhani Yehoyada akaweka uangalizi wa Hekalu la BWANA mikononi mwa makuhani, waliokuwa Walawi, ambao Mfalme Daudi alikuwa amewagawa ili wahudumu hekaluni kwa ajili ya kutoa sadaka za kuteketezwa za BWANA kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, kwa kushangilia na kuimba kama Daudi alivyokuwa ameagiza. 19Pia akawaweka mabawabu kwenye malango ya Hekalu la BWANA ili kwamba kwa vyo vyote asije akaingia mtu ye yote aliye najisi.

20Akawachukua majemadari wa mamia, watu waheshimiwa, viongozi wa watu pamoja na watu wote wa nchi na kumteremsha mfalme kutoka hekaluni mwa BWANA. Wakaingia kwenye jumba la kifalme kwa kupitia Lango la Juu na kumkalisha mfalme kwenye kiti cha enzi cha ufalme, 21nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga.

Copyright information for Neno