2 Corinthians 10

Paulo Atetea Huduma Yake

1Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi! 2Nawaomba nitakapokuja kwenu nisiwe na ujasiri dhidi ya watu fulani, kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata namna ya ulimwengu huu. 3Ingawa tunaishi duniani lakini hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. 4Silaha za vita vyetu si za mwili, Bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome. 5Tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo, 6tena tukiwa tayari kuadhibu kila tendo la kutokutii, kutii kwenu kutakapokamilika.

7Angalieni yale yaliyo machoni penu. Kama mtu ye yote anaamini kuwa yeye ni mali ya Kristo, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Kristo, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo. 8Basi hata kama nikijisifu zaidi kidogo kuhusu mamlaka tuliyo nayo, ambayo Mungu alitupa ili kuwajenga wala si ya kuwabomoa, mimi sitaionea haya. 9Sitaki nionekane kama ninayejaribu kuwatisha kwa nyaraka zangu. 10Kwa maana wanasema, “Nyaraka zake ni nzito na zenye nguvu, lakini akiwepo kwa mwili ni dhaifu na kuzungumza kwake ni kwa kudharauliwa.” 11Watu kama hao wajue ya kuwa, yale tusemayo kwa barua tukiwa hatupo pamoja nanyi, ndivyo tulivyo na ndivyo tutakavyofanya tutakapokuwa pamoja nanyi.

12Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonyesha ya kuwa hawana busara. 13Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi. 14Kwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama vile ambavyo ingekuwa kama hatukuwa tumekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Kristo. 15Wala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi, 16ili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine. 17Lakini, “yeye ajisifuye ajisifu katika Bwana.” 18Kwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Bwana humsifu.

Copyright information for Neno