2 Corinthians 11

Paulo Na Mitume Wa Uongo

Laiti mngechukuliana nami kidogo katika upumbavu wangu! Naam, chukulianeni nami. Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi. Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo. Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi. Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu.” Inawezekana mimi nikawa si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.

Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo? Niliyanyang'anya makanisa mengine kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi. Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nikipungukiwa na cho chote, sikuwa mzigo kwa mtu ye yote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walinipatia mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yo yote, nami nitaendelea kujizuia. 10 Kwa hakika kama vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu ye yote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili. 11 Kwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda! 12 Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.

13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo. 14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 15 Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.

Paulo Anajivunia Mateso Yake

16 Nasema tena, mtu ye yote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata kama mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo. 17 Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi kama vile ambavyo Bwana angesema, bali kama mjinga. 18 Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu. 19 Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana! 20 Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida au akiwanyang'anya au akijitukuza mwenyewe au akiwadanganya. 21 Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo!

Lakini cho chote ambacho mtu mwingine ye yote angethubutu kujisifia, nanena kama mjinga, nami nathubutu kujisifu juu ya hilo.
22 Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Abrahamu? Mimi pia ni mzao wa Abrahamu. 23 Je, wao ni watumishi wa Kristo? Nanena kiwazimu, mimi ni zaidi yao: Nimefanya kazi kwa bidii kuliko wao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimechapwa mijeledi sana, nimekabiliwa na mauti mara nyingi. 24 Mara tano nimechapwa na Wayahudi viboko arobaini kasoro kimoja. 25 Mara tatu nalichapwa kwa fimbo, mara moja nalipigwa kwa mawe, mara tatu nimevunjikiwa na meli, nimekaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa, 26 katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyang'anyi, hatari kutoka kwa watu wangu mwenyewe, hatari kutoka kwa watu Mataifa, hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini, hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. 27 Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi, ninajua kukaa njaa na kuona kiu, nimekaa mara nyingi bila chakula, nimesikia baridi na kuwa uchi. 28 Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa na mzigo wa wajibu wangu kwa makanisa yote. 29 Je, ni nani aliye dhaifu, nami nisijisikie dhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike?

30 Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonyesha udhaifu wangu. 31 Mungu na Baba wa Bwana Yesu, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo. 32 Huko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata. 33 Lakini nilishushwa kwa kapu kubwa kupitia katika dirisha ukutani, nikatoroka kutoka mikononi mwake.

Copyright information for Neno