2 Kings 24

Wakati wa utawala wa Yehoiakimu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliishambulia nchi, naye Yehoiakimu akawa mtumwa wake kwa miaka mitatu. Lakini hatimaye akabadili mawazo yake na kuasi dhidi ya Nebukadneza. BWANA akatuma Wakaldayo, Waaramu, Wamoabu na Waamoni ili kumshambulia ghafula. Aliwatuma kuiangamiza Yuda sawasawa na neno la BWANA lililosemwa na watumishi wake manabii. Hakika mambo haya yalitokea Yuda kulingana na agizo la BWANA, ili kuwaondoa kutoka machoni pake kwa sababu ya dhambi za Manase na yote aliyoyafanya, ikiwa ni pamoja na kumwaga damu isiyo na hatia. Kwa kuwa aliijaza Yerusalemu kwa damu isiyo na hatia na BWANA hakuwa radhi kusamehe.

Matukio mengine ya utawala wa Yehoiakimu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda? Yehoiakimu akalala pamoja na baba zake. Naye Yehoyakini mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Mfalme wa Misri hakutoka tena katika nchi yake, kwa sababu mfalme wa Babeli alikuwa ameitwaa himaya yake yote, kuanzia Kijito cha Misri hadi Mto Eufrati.

Yehoyakini Mfalme Wa Yuda

Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa miezi mitatu. Jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani kutoka Yerusalemu. Akafanya maovu machoni pa BWANA, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.

10 Wakati huo, maafisa wa Nebukadneza mfalme wa Babeli walikuja ili kuishambulia Yerusalemu nao wakaizunguka kwa jeshi. 11 Nebukadneza mwenyewe akaupandia mji wakati maafisa wake walipokuwa wameuzunguka kwa jeshi. 12 Yehoyakini mfalme wa Yuda, mama yake, wahudumu wake, wakuu na maafisa wake wote wakajisalimisha kwa Nebukadneza.

Katika mwaka wa nane wa utawala wa mfalme wa Babeli, akamchukua Yehoyakini kuwa mfungwa.
13 Kama vile BWANA alivyokuwa amesema, Nebukadneza akaondoa hazina yote kutoka Hekalu la BWANA na kutoka jumba la mfalme, akavichukua vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Solomoni mfalme wa Israeli alikuwa amevitengeneza kwa ajili ya Hekalu la BWANA. 14 Akawachukua Yerusalemu wote kwenda uhamishoni: yaani, maafisa wote na mashujaa, watu wenye ustadi na ufundi, jumla yao watu elfu kumi. Watu maskini sana ndio tu waliobaki katika nchi.

15 Nebukadneza akamchukua mateka Yehoyakini kwenda Babeli. Pia akawachukua utumwani kutoka Yerusalemu kwenda Babeli mama yake mfalme, wake zake, maafisa wake na viongozi wote wa nchi. 16 Mfalme wa Babeli pia akawahamishia Babeli mashujaa elfu saba, wenye nguvu na wanaofaa kupigana vita, watu wenye ustadi na mafundi elfu moja. 17 Akamfanya Matania, ndugu wa baba yake Yehoyakini, kuwa mfalme mahali pake na akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia.

Sedekia Mfalme wa Yuda

18 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake aliitwa Hamuthi binti Yeremia, kutoka Libna. 19 Akafanya maovu machoni mwa BWANA, kama alivyofanya Yehoiakimu. 20 Ilikuwa ni kwa sababu ya hasira ya BWANA haya yote yakatokea katika Yerusalemu na katika Yuda, na mwishoni akawasukumia mbali na uso wake.

Kuanguka Kwa Yerusalemu

Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli.

Copyright information for Neno