2 Kings 8

Ardhi Ya Mshunami Yarudishwa

Wakati huu, Elisha alikuwa amemwambia yule mwanamke ambaye mwanawe alikuwa amefufuliwa, “Ondoka wewe na jamaa yako ukaishi mahali po pote unapoweza kwa kitambo kidogo, kwa sababu BWANA ameamuru njaa katika nchi hii ambayo itadumu kwa miaka saba.” Yule mwanamke akafanya kama vile yule mtu wa Mungu alivyosema. Yeye na jamaa yake wakaondoka na kwenda kuishi katika nchi ya Wafilisti kwa miaka saba.

Baada ya miaka saba yule mwanamke akarudi kutoka nchi ya Wafilisti na kwenda kwa mfalme kumwomba kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake. Mfalme alikuwa anazungumza na Gehazi, mtumishi wa mtu wa Mungu, naye alikuwa amesema, “Hebu niambie mambo yote makuu yaliyofanywa na Elisha.” Wakati Gehazi alipokuwa akimweleza mfalme jinsi Elisha alivyomfufua mtu, yule mwanamke ambaye mwanawe alikuwa amefufuliwa na Elisha akaja ili amwombe mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake.

Gehazi akasema, “Huyu ndiye huyo mwanamke, bwana wangu mfalme, na huyu ndiye mwanawe ambaye Elisha alimfufua.”
Mfalme akamwuliza yule mwanamke kuhusu mambo hayo, naye akamweleza.

Ndipo akaamuru afisa ashughulikie shauri lake na kumwambia, “Mrudishie huyu mwanamke kila kitu kilichokuwa mali yake, pamoja na mapato yote yaliyotokana na shamba lake tangu siku alipoondoka nchini hadi sasa.”

Hazaeli Anamwua Ben-Hadadi

Elisha akaenda Dameski, naye Ben-Hadadi mfalme wa Aramu alikuwa mgonjwa. Mfalme alipoambiwa, “Mtu wa Mungu ametoka mbali akapanda hadi hapa,” mfalme akamwambia Hazaeli. “Chukua zawadi na uende kumlaki huyo mtu wa Mungu. Mwulize BWANA kupitia yeye, kwamba, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’ ”

Hazaeli akaenda kumlaki Elisha, akiwa amechukua kila kitu kizuri kilichopatikana Dameski, mizigo iliyobebwa na ngamia arobaini. Akaingia ndani na kusimama mbele yake, akasema, “Mwanao Ben-Hadadi mfalme wa Aramu amenituma niulize, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’ ”

10 Elisha akajibu, “Nenda ukamwambie, ‘Hakika utapona’; lakini BWANA amenifunulia kwamba kweli atakufa.” 11 Elisha akamkazia Hazaeli macho kwa nguvu mpaka akaona aibu. Kisha mtu wa Mungu akaanza kulia.

12 Hazaeli akauliza “Kwa nini bwana wangu analia?”

Elisha akajibu, “Kwa sababu najua mabaya utakayowatendea Waisraeli. Utachoma moto ngome zao, utawaua vijana wao kwa upanga, kuwatupa chini kwa nguvu watoto wachanga na kuwatumbua wanawake wenye mimba.”

13 Hazaeli akasema, “Itawezekanaje mtumishi wako, aliye mbwa tu, kufanya tendo la ajabu namna hiyo?”

Elisha akamjibu, “BWANA amenionyesha kuwa utakuwa mfalme wa Aramu.”

14 Kisha Hazaeli akamwacha Elisha na kumrudia bwana wake. Ben-Hadadi akamwuliza, “Elisha alikuambia nini?” Hazaeli akajibu, “Aliniambia kwamba hakika utapona.” 15 Lakini kesho yake Hazaeli akachukua nguo nzito, akailoweka ndani ya maji, akaitandaza juu ya uso wa mfalme, hivyo akafa. Kisha Hazaeli akaingia mahali pake kuwa mfalme wa Aramu.

Yehoramu Mfalme Wa Yuda

16 Katika mwaka wa tano wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, wakati huo Yehoshafati akiwa mfalme wa Yuda, Yehoramu mwana wa Yehoshafati akaanza kutawala kama mfalme wa Yuda. 17 Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa miaka minane. 18 Akaziendea njia za wafalme wa Israeli, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alimwoa binti wa Ahabu. Akatenda maovu machoni pa BWANA. 19 Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi mtumishi wake, BWANA hakutaka kuiangamiza Yuda. Alikuwa ameahidi kuidumisha taa kwa ajili ya Daudi na uzao wake milele.

20 Wakati wa Yehoramu, Edomu waliasi dhidi ya Yuda na kuweka mfalme wao wenyewe. 21 Basi Yehoramu akaenda Seiri pamoja na magari yake yote ya vita. Waedomu wakamzunguka pamoja na jemadari wake wa jeshi wa magari ya vita. Lakini akaondoka usiku na kuwashambulia Waedomu waliokuwa wamemzunguka, hata hivyo, jeshi lake likakimbia kurudi nyumbani. 22 Mpaka leo Edomu wamekuwa waasi dhidi ya Yuda. Libna pia wakaasi wakati huo huo.

23 Kwa matukio mengine ya utawala wa Yehoramu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda? 24 Yehoramu akalala pamoja na baba zake na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Naye Ahazia mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Ahazia Mfalme Wa Yuda

25 Katika mwaka wa kumi na mbili wa kutawala kwake Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alianza kutawala. 26 Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili wakati alipokuwa mfalme, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Jina la mama yake ni Athalia, mjukuu wa Omri mfalme wa Israeli. 27 Akaziendea njia za nyumba ya Ahabu na kutenda maovu machoni pa BWANA, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alikuwa ameoa kutoka nyumba ya Ahabu.

28 Ahazia akaenda vitani na Yoramu mwana wa Ahabu dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu. 29 Basi Mfalme Yoramu akarudi Yezreeli ili apate kutibu majeraha aliyoyapata huko Ramoth
8.29 Yaani Rama kwa Kiebrania
alipokuwa anapigana na Hazaeli mfalme wa Aramu.

Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda, akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.

Copyright information for Neno