2 Peter 3

Ahadi Ya Kuja Kwa Bwana

1Wapenzi, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha kwamba, 2nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa kupitia kwa mitume wenu.

3Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbaya, 4wakisema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipokufa, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” 5Wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa hayo maji, 6ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa na kuangamia. 7Lakini kwa neno lilo hilo mbingu za sasa na dunia, zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.

8Lakini wapenzi, msisahau neno hili, kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu na miaka elfu ni kama siku moja. 9Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake kama watu wengine wanavyodhani kukawia. Yeye anawavumilia, maana hataki mtu ye yote aangamie, bali kila mmoja afikilie toba.

10Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu na vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.

11Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, ninyi je, imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu, ambayo siku hiyo mbingu zitachomwa moto na kutoweka na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. 13Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia kwa furaha mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.

14Kwa sababu hii, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia kwa furaha mambo haya, fanyeni bidii ili awakute katika amani, bila mawaa wala dosari. 15Nanyi hesabuni uvumilivu wa Bwana kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu. 16Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha kwa maangamizi yao wenyewe, kama wapotoshavyo pia Maandiko mengine.

17Basi, ninyi wapenzi, kwa kuwa mmekwisha kujua mambo haya, jilindeni msije mkachukuliwa na kosa la watu hao waasi na kuanguka kutoka kwenye uthabiti wenu. 18Bali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na milele! Amen.

Copyright information for Neno